Mradi wa umeme Rufiji MW 2,100 kuanza Machi

MRADI wa Kuzalisha Umeme Rufiji (RHPP) wenye uwezo wa kufua megawati 2,100, utaanza kutekelezwa Machi mwaka huu, imefahamika.

Kauli hiyo ilitolewa na mhaidolojia wa mradi huo, Stanislaus Kizzy katika mkutano kuhusu RHPP na Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini pamoja na wabunge wa mikoa ya Morogoro, Njombe, Iringa na Pwani.

Kizzy alisema mradi huo utakapokamika katika kipindi cha miezi 36, bwawa hilo litakuwa na mita za ujazo bilioni 35 katika ujazo wake wa juu na kontua ya mita 188 pamoja na mita za mraba 914.

Mhaidolojia huyo alisema bwawa hilo litakuwa na urefu wa kilometa 100 na upana wa kilometa 25 na litaongeza upatikanaji wa maji kwa ajili ya wanyama na kuwapunguzia umbali na ugumu wa kufuata maji mbali mtoni hasa wakati wa kiangazi.

Aidha, visima vitakavyotokana na bwawa vitakuwa na faida kubwa katika Ikolojia ya Selous kwa kutengeneza mazingira mazuri ya mazalia ya samaki na wanyama waishio majini. Kizzy alisema bwawa litarahisha usafiri wa askari na wahifadhi wa Selous na kuwezesha sehemu zilizokuwa hazifikiki wakati wa mashika kufikika.

Akifafanua kuhusu mradi huo, Mhandisi John Mageni alisema mradi wa kuzalisha umeme Rufiji utajengwa katika mto Rufiji, sehemu ambayo mto unakata mpaka wa Mkoa wa Morogoro na Pwani katika Wilaya ya Rufiji.

Mageni alisema eneo la kidakia maji cha mradi wa umeme wa Rufiji ni kilometa za mraba 158,420 na mradi huo unahusisha mikoa 10 ya Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Mbeya, Njombe, Iringa, Ruvuma na Lindi.

“Mradi huo utahusisha wilaya 30 za Chunya, Iringa Vijjini, Iringa Mjini, Njombe Mjini, Njombe, Tunduru, Mbeya, Mbeya Mjini, Mpwapwa, Bahi, Mufindi, Songea, Wanging’ombe, Makete, Manyoni, Chamwino, Kilolo, Liwale, Rungwe, Sikonge, Malinyi, Ulanga, Dodoma Mjini, Ikungi, Namtumbo, Rufiji, Mbarali, Morogoro, Kilombero na Kilosa,” alisema Mageni.

Mradi huo utahusisha pia mbuga za wanyama saba za Selous, Mikumi, Mlima Udzungwa, Ruadha, Rungwa na Mhesi na utakuwa na uhakika wa upatikanaji wa maji kwa ajili ya mradi wa Rufiji unategemea sana matumizi bora ya maji katika mikoa na wilaya tajwa.

Lakini pia alisema utahusiha majimbo ya uchaguzi 35 ya Bahi, Dodoma Mjini, Ileje, Iringa Mjini, Ismani, Kalenga, Kibakwe, Kilolo, Kilombero, Kilosa, Liwale, Lupa, Lupembe, Madaba, Makambako, Makete, Malinyi, Manyoni Magharibi, Manyoni Mashariki, Mbarali, Mbeya Mjini, Mbeya Vijijini, Mlimba na Morogoro Kusini.

Mengine ni Mpwapwa, Mtera, Mufindi Kaskazini, Mufindi Kusini, Namtumbo, Njombe Mjini, Rufiji, Sikonge, Tunduru Kaskazini, Ulanga, Wanging’ombe na katika kata 248.

Awali akielezea mradi huo, Waziri wa Nishati, Dk Merard Kalemani alisema utekelezaji wa mradi huo ambao umekuwa ukisemwa kwamba wa kuzalisha umeme wa maji kutokana katika maporomoro ya Mto Rufiji, zamani uliitwa Stiegler’s Gorge, lakini unaitwa Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Maji katika Mto Rufiji.

Dk Kalemani alisema mradi huo uchunguzi wake ulianza tangu miaka 1970, haukuweza kutekelezeka, lakini mwaka jana serikali ikaamua kuutekeleza. “Mradi huo ni injini kubwa katika kujenga uchumi wa viwanda.

Tunao umeme wa kutosha kwa sasa wa megawati 1,451 kwenye gridi na hivyo kuongeza, megawati 2,100, ni kuongeza nguvu kubwa ya nishati hiyo,” alisema. Alisema maandalizi ya awali yamefanyika, zabuni zilishafunguliwa juzi (kampuni tano zimejitokeza) na msimamizi ni serikali, na tayari timu imeundwa kuhakikisha mradi huo unafanyika kwa haraka.

Source: www.habarileo.co.tz