Mbowe, Polepole wamjibu Zitto kusitisha kampeni

Chama cha Mapinduzi (CCM), kimesema kipindi hiki cha msiba wa mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru ndicho cha kuvieleza vyama vinavyoshiriki uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo ya Siha na Kinondoni kufanya kampeni safi.

Wakati chama hicho kikisema hayo kupitia kwa katibu wake wa itikadi na uenezi, Humphrey Polepole, chama kingine kinachoshiriki kampeni hizo, Chadema kimesema kitasimamisha shughuli zote za kampeni Jumatatu siku ambayo mwanasiasa huyo atazikwa katika makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Kauli ya vyama hivyo imetokana na wito uliotolewa na Kiongozi wa Chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe kwa vyama hivyo kusimamisha kampeni hizo kwa siku tatu kuomboleza kifo cha mwanasiasa huyo mkongwe nchini kutokana na mchango wake katika siasa za nchi na zaidi ndani ya vyama hivyo. “Kingunge amesaidia kuimarisha CCM na baadaye akasaidia Chadema. Sioni busara vyama kuendelea na kampeni. Nawaomba wasitishe leo (jana), kesho (leo) na Jumatatu mwanasiasa huyu akizikwa wataendelea,” alisema jana nyumbani kwa marehemu, Kijitonyama, Dar es Salaam.

Alipoulizwa kuhusu wito huo, Polepole alisema kwa kuwa mwanasiasa huyo ameishi na kufa akiamini katika siasa za ujamaa na kujitegemea ambazo msingi wake ni kufanya kazi, huu si wakati wa kusimamisha kampeni. “Ni wakati wa kueleza kuwa vyama vya siasa vina jukumu la kufanya kampeni safi, kujenga misingi imara ya kuwapata makada na wanachama wanaosimamia kwenye imani ya vyama vyao na kuwapata viongozi bora.” Alisema kazi kubwa aliyoifanya Kingunge tangu kuasisiwa kwa Taifa hadi alipofariki, inapaswa kuendelezwa. “Nanukuu kifungu cha Biblia ‘mbio amezipiga na mwendo ameumaliza’. Hivyo Kingunge ameumaliza mwendo kazi kubwa ni kuendeleza mema na mazuri aliyotenda,” alisema Polepole.

Mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano, uenezi na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu ombi hilo la Zitto alisema chama hicho kitasitisha kampeni zake kesho. “Huu ni ushauri, na mzee wetu amefariki dunia kampeni zikiwa zimeanza na zinafanyika kwa muda mfupi kabla ya uchaguzi. Tuliona Jumatatu (kesho) ndio tushiriki kikamilifu kumuaga mzee wetu na hatutafanya kampeni.”

Hata hivyo, Mrema alisema awali kwamba ni vigumu kutoa uamuzi kuhusu ushauri huo wa Zitto kwa kuwa suala hilo linapaswa kutolewa tamko baada ya vikao kauli inayofanana na ya mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe. “Leo (jana) baada ya kampeni tutafanya kikao cha tathmini lakini ni kwamba sisi tuliona Jumatatu kuwa siku muafaka kutofanya kampeni ili kushiriki shughuli ya kumhifadhi mzee wetu,” alisema Mrema huku Mbowe akisema, “Hili ni swali gumu, lakini nitakwenda kushauriana na viongozi ili tujue cha kufanya.”

Vyama takriban 12 vipo katika kampeni za ubunge jimbo la Kinondoni, Dar es Salaam na Siha, Kilimanjaro zilizoanza Januari 21 zikitarajiwa kumalizika Februari 16 huku uchaguzi katika majimbo hayo na kata 10 ukitarajiwa kufanyika Februari 17.

Kingunge aliyekuwa kada wa CCM mwenye kadi namba nane, alitangaza kukihama chama hicho Oktoba 4, 2015 na kusema hatajiunga na chama chochote lakini mara kadhaa alionekana akipanda majukwaa ya upinzani kumnadi aliyekuwa mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015.

Mwanasiasa huyo alifariki dunia juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ikiwa ni mwezi mmoja baada ya mkewe, Peras kufariki katika hospitali hiyohiyo.

Ndiye aliyebuni umoja wa vijana
Akimzungumzia marehemu Kingunge, Balozi wa Tanzania nchini Brazil, Dk Emmanuel Nchimbi ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa UVCCM alisema mwanasiasa huyo ndiye aliyeanzisha wazo la kuanzishwa kwa umoja wa vijana wa Tanu na baadaye kuwa katibu mkuu wake wa kwanza. “Nimefanya kazi na Mzee Kingunge nikiwa Mwenyekiti wa UVCCM na yeye akiwa Kamanda na Naibu Kamanda Mkuu wa UVCCM kwa miaka 10.

Alikuwa kamanda na mlezi wa kweli wa vijana. Mara zote nilimfahamu kama mtu anayependa nchi na chama kwa kiwango cha hali ya juu,” alisema Dk Nchimbi na kuongeza; “Mwaka 2000, UVCCM tulifanya mazungumzo na hayati Mzee Kawawa na tukampongeza kwa kuanzisha Tanu Youth League (Umoja wa Vijana wa Tanu). Mzee Kawawa akatuambia aliyenipa wazo la kuanzisha Youth League alikuwa ni Mzee Kingunge na ndicho kilichofanya ateuliwe kuwa katibu mkuu wa kwanza wa Umoja wa Vijana wa Tanu. Mzee Kawawa akatuambia kuwa wazo la kuunganisha Tanu na ASP lilitolewa kwa mara ya kwanza na Tanu Youth League. Kwa hiyo mchango wa Mzee Kingunge katika historia ya nchi yetu una nafasi kubwa sana na ni wa kipekee.”

CCM yatuma salamu za rambirambi
Katika salamu zake kuhusiana na kifo cha mwanasiasa huyo, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema chama hicho tawala kitamkumbuka Kingunge kama mmoja wa raia mashuhuri ambaye ameshiriki harakati za uhuru na Muungano wa Taifa na kwamba alikuwa sehemu ya Umoja wa Vijana wa Tanu waliokuwa mstari wa mbele katika kupigania ukombozi wa Taifa. “Hata wakati tunalisuka upya jeshi jipya la nchi yetu, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na baadaye Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mzee Ngombale alikuwa mojawapo ya makamisaa wa chama waliohusika kutoa elimu ya siasa jeshini,” alisema.

Katika salamu hizo, Polepole alisema, “Chama cha Mapinduzi kinaamini kujikwaa sio kuanguka na mara zote dhamira njema na ya dhati hushinda, Mzee Ngombale Mwiru ametangulia mbele ya haki akiwa mwana CCM kwelikweli.”

Source: http://www.mwananchi.co.tz