Magufuli ataka Airtel kurejeshwa serikalini

RAIS John Magufuli amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango kufuatilia Kampuni ya Simu ya Mkononi ya Airtel ili kujua ukweli ili umiliki wake urudi serikalini kabla ya kuisha kwa mwaka huu.

Alisema hayo jana katika hafla ya kuweka jiwe la msingi la jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inayojengwa katika eneo la Makulu mjini hapa. Rais Magufuli alimuagiza Waziri wa Fedha na Mipango kufuatilia suala hilo haraka ili Airtel irudishwe kumilikiwa na serikali. “Fuatilia suala la Airtel, Airtel kwa taarifa tulizonazo ni mali ya TTCL (Kampuni ya Simu Tanzania).

Palifanyika mchezo wa hovyo, sasa sitaki kuzungumza mengi fuatilia. “Nchi hii ilikuwa ya maajabu sana unachukua share (hisa) leo, kesho inauzwa, kisha zinafutwa na kuuzwa juu kwa dola moja,” alisema Rais Magufuli. Taarifa kuhusu Airtel Taarifa za kuaminika kutoka serikalini, zinaeleza kuwa TTCL itamiliki hisa zote za Airtel Tanzania Limited, ambapo tayari TTCL imewasilisha hoja ya kutaka kufanya hivyo baada ya kubaini kwamba serikali ilipunjwa kwenye hesabu za uwekezaji.

Inaelezwa kuwa hoja ya Airtel kuwa mali ya TTCL inaanzia Novemba 3, 1998, ilipoanzisha kampuni tanzu ya Cellnet ambayo ilifanya kazi mpaka Mei 7, 2001 ilipobadilishwa jina na kuitwa Celtel Tanzania, huku umiliki wake ukiendelea kuwa chini ya shirika hilo kwa asilimia zote baada ya kuwekeza dola milioni tano za Marekani (zaidi ya Shbilioni 11). Inaelezwa kuwa Januari 31, 2002, Celtel ikiwa chini ya umiliki wa TTCL ilikopa dola 82 milioni (zaidi ya Sh bilioni 180.4) ili kukuza mtaji wake.

Kwa kipindi hicho, TTCL iliyokuwa na thamani ya dola 600 milioni (zaidi ya Sh trilioni 1.32) ilikuwa inamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali na Kampuni ya Mobile System International (MSI) ya Uholanzi. Serikali ilikuwa inamiliki asilimia 65 ya hisa zote na mbia huyo asilimia 35 zilizosalia. Agosti 5, 2005, mabadiliko yalifanywa kwenye Bodi ya Wakurugenzi wa Celtel kwa lengo la kuunda kampuni mbili tofauti; Celtel ikatenganishwa na TTCL.

Kutokana na mabadiliko hayo, Celtel iliwekwa chini ya umiliki wa MSI ambayo Septemba 2007 iliuza hisa zake kwa Zain, ambayo nayo ilikuja kuziuza kwa Bharti Airtel Juni 8, 2010. Imeelezwa kuwa TTCL inadai uwekezaji wake ilioufanya Celtel baadaye Airtel, ambayo thamani yake imeongezeka maradufu sasa, haulingani na inachokipata, hivyo kutaka kusimamia biashara za kampuni hiyo ya mawasiliano.

Hoja ya madai hayo ni namna umiliki wa hisa ulivyobadilishwa baada ya Celtel kutenganishwa na TTCL, ambayo ilipewa hisa chache, tofauti na ilivyostahili. Kwa sasa, Airtel Tanzania inamilikiwa na Serikali yenye asilimia 40 na Celtel Tanzania BV, kampuni tanzu ya Zain Africa BV ambayo ilinunuliwa na Bharti Airtel International, Novemba, 2010 ikiwa na asilimia 60.

Katika mabadiliko yaliyofanywa hivi karibuni, Serikali iliilipa Bharti Airtel Sh bilioni 14.7 hivyo kuchukua asilimia 35 ya hisa ilizokuwa inamiliki na kuifanya imiliki asilimia zote za TTCL. Sheria mpya iliyopitishwa hivi karibuni na Bunge, imeibadili TTCL inayohudumia asilimia 0.82 ya soko kuwa shirika la umma la mawasiliano na kulipa jukumu kubwa katika sekta ya mawasiliano nchini.

Bharti Airtel inatakiwa kuorodhesha asilimia 25 ya hisa zake katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) ili kukidhi vigezo vya Sheria ya Posta na Mawasiliano ya mwaka 2010, lakini haijafanya hivyo. Onyo kwa watoa takwimu za uongo Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ametoa onyo kuwa hatua kali zitachukuliwa na mamlaka husika kwa mtu yeyote atakayetoa takwimu za uongo kwa lengo la kupotosha umma.

Alisema kwa mujibu wa Kifungu cha Sheria 37 ya Mwaka 2015 Namba 3 hadi 5, adhabu kali zitachukuliwa kwa mtu atayehusika kutoa taarifa za uongo, ikiwa ni pamoja na kufungwa jela miezi sita au miaka mitatu au kulipa faini ya Sh milioni moja au adhabu zote kwa pamoja. “Nawaomba Watanzania, kwa mtu yeyote atayehitaji takwimu za kitu chochote, akachukue kwa mamlaka husika,” aliagiza Rais Magufuli.

Pia alisema uchumi wa Tanzania unakua, ambapo katika nusu ya kwanza ya mwaka huu umekua kwa asilimia 6.8, mfumuko wa bei umeshuka hadi kufikia asilimia 4.4 mwezi Novemba 2017 na akiba ya fedha za kigeni imefikia dola za Marekani bilioni 5.82, ambayo inaiwezesha nchi kununua bidhaa na huduma miezi mitano, ikilinganishwa na wastani unaopaswa wa miezi minne.

“Mpaka sasa Tanzania imeweka Sh bilioni 5.8 ya akiba ya fedha za kigeni na Sh bilioni 2.5 zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya vituo vya mkoa wa Dodoma,” alisema. Alisema pia kwa muda wa miaka miwili, jumla ya viwanda vipya 336 vimejengwa. “Serikali imetenga kiasi cha Sh bilioni 23 kwa kila mwezi kwa ajili ya kutoa elimu bure na mpaka sasa asilimia 31 ya wanafunzi hujiunga na kidato cha kwanza,” alisema Rais Magufuli.

Pia aliwataka Watanzania kupuuza msemo wa kuwa ‘vyuma vimekaza’, badala yake kuangalia takwimu zinasema nini kuhusu uchumi wa Taifa. “Kwa wale wanaolalamika vyuma vinabana, wajue vitaendelea kubana tumbo, vitabana kichwa na hata viungo vyote vya mwili,” alisema Rais Magufuli. Awali, akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Twakimu (NBS), Dk Albina Chuwa alisema kwa mujibu wa takwimu za Taifa, matarajio ya mwaka 2022, idadi ya Watanzania itaongezeka mpaka kufikia milioni 61.3.

“Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika baada ya Afrika Kusini katika ukusanyaji wa takwimu bora, tumeendelea kutoa mafunzo kwa watakwimu katika taasisi za serikali ili kuendana na mabadiliko katika eneo la takwimu,” alisema.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mpango alisema ujenzi wa ofisi hizo ni agizo la Rais Magufuli la kuhamisha shughuli za serikali Makao Makuu Dodoma. Msomi azungumzia hisa za Airtel Kutokana na agizo hilo la Rais Magufuli kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mpango, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Bana alisema linapaswa kuungwa mkono.

Alisema kumekuwa na michezo ya hovyo kwa miaka ya hivi karibuni kwa baadhi ya makampuni na mahoteli, kubadilisha majina kinyemela, hali inayoleta wasiwasi kwamba ni moja ya njia za ukwepaji kodi.

Profesa Bana alisema kuwa Rais anavyo vyombo vyake, ambavyo vinampa taarifa nyingi, hivyo maagizo yake kwa Waziri wa Fedha ni sahihi. Kwa upande mwingine, baadhi ya wachumi waliozungumza na gazeti hili walisema hawawezi kutoa maoni yoyote, kwa kuwa agizo hilo linamtaka Waziri kulifanyia kazi. Walisema kwa kuwa suala lenyewe, pia ni la kimikataba na la kisheria, hivyo ingefaa watu wawe na uvumilivu, kuona ni kitu gani Dk Mpango aliyeagizwa kufuatilia, atakuja nacho.

Source: www.habarileo.co.tz