Wasambaza uongo Bakwata kukiona

BARAZA Kuu la Waislamu nchini (Bakwata) Mkoa wa Dar es Salaam limesema kuwa watu wote waliosambaza taarifa za uongo na uchochezi kuhusu Mufti na Shehe Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir pamoja na baraza hilo watachukuliwa hatua kwa kuwa wanafahamika.

Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Shehe Mkuu wa Mkoa huo, Alhad Mussa Salum wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa hizo zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari. Kauli hiyo imekuja baada ya hivi karibuni katika mitandao mbalimbali ya kijamii ilisambaa taarifa kuwa mfumo wa baraza hilo kiutendaji hauko imara na wana mkakati wa kumpindua Zubeir.

“Kwa hakika tunawajua hawa ambao wamelianzisha hili na Mufti anawajua na mimi ninawajua na mufti atawashughulikia hivi karibuni kwa kuwa waliotengeneza ni watu wachache waliomo ndani ya baraza,” alisema Salum.

Alisema Waislamu kote nchini wanapaswa kupuuza taarifa hizo kwa kuwa ni za uongo na zina lengo la kudhoofisha baraza na jitihada za Mufti za kuokoa na kuzilinda mali za baraza na kulijenga upya ili liweze kujitegemea na kujiendesha lenyewe kiuchumi na kuwaunganisha Waislamu wote nchini kuwa kitu kimoja bila kujali tofauti zao kiitikadi.

“Hakuna shehe yeyote kwetu sisi mashehe wa mikoa kama wasaidizi wake ambaye hana imani na mufti kama inavyodaiwa na hakuna mjumbe yeyote wa Baraza la Ulamaa ambaye hana imani na mufti wala mashehe wa wilaya hasa ukizingatia kwa muda mfupi mambo ambayo ameyafanya,” aliongeza. Aidha, Salum alisema kuwa Bakwata ni baraza ambalo linajitegemea na siyo tawi la Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama taarifa mbalimbali katika mitandao ya kijamii zinavyodai.

Source: www.habarileo.co.tz