Mshambuliaji wa Vital’O asaini Stand United

Shinyanga.
Stand United “Chama la Wana” katika kuhakikisha inajinasua kutoka mkiani kwa kumnasa mshambuliaji wa  Vital’O ya Burundi, Ndikumana Selemani.

Stand United imeanza vibaya Ligi Kuu ikiwa moja ya timu tatu za mwisho huku tatizo lao kubwa likiwa ni safu ya ushambuliaji.
Katika kuhakikisha tatizo hilo linakwisha uongozi wa timu hiyo umemsajili mshambuliaji huyo Mrundi bila ya kuweka wazi amesaini mkataba wa miaka mingapi.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Agustino Malindi alisema tayari mshambuliaji huyo ameshatua  Shinyanga.

“Tunawashukuru viongozi wetu kwa kufanikisha hili dili kwani huyo mchezaji ni bonge la mshambuliaji,”alisema Malindi.

Hata hivyo kocha huyo alisema lengo lao ni kuongeza washambuliaji wanne ili kumaliza tatizo la umaliziaji ndani ya kikosi chao.

Mwenyekiti wa timu hiyo, Dk Elyson Maheja alisema wanataka kuona klabu hiyo inafanya vyema katika ligi hiyo.

“Tutaongeza nguvu ndani ya timu hiyo kwani ipo katika nafasi mbaya kwenye msimamo wa Ligi Kuu hivyo ni lazima tupambane ili tuweze kupata matokeo mazuri,”alisema Maheja.

Source: http://www.mwanaspoti.co.tz